Dkt Mwakyembe; Cheneli ya Utalii itasaidia katika kukuza na kutangza sekta ya Utalii Nchini.


Imewekwa 16th November, 2018

Waziri wa Habari utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Chaneli ya Utalii itakayokuwa ikirushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), italenga katika kukuza utalii nchini kwa kutangaza vivutio vilivyopo ikiwemo mbuga za wanyama,Utamaduni pamoja na uoto wa asili.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dodoma katika kikao cha pamoja cha Mawaziri wanaohusika na sekta ya mawasiliano,utalii, mifugo na kilimo na habari ambapo Bw.Gabriel Nderumaki aliwasilisha taarifa fupi ya Mradi wa uanzishwaji wa Chaneli hiyo itakayojulikana kama “Tanzania Safari Chaneli”.

Akiwasilisha taarifa hiyo alieleza kuwa Chaneli hiyo itakuwa inarusha matangazo kwa muda wa saa ishirini na nne kwa siku kutokea studio ya mikocheni Jijini Dar es Salaam kuanzia mwezi Disemba.

Akichangia mawazo baada ya Uwasilishaji wa Taarifa hiyo Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameeleza kuwa matangazo ya chaneli hiyo ni vyema yakawa katika lugha ya Kiswahili ili kukuza lugha hiyo ambayo ndio utambulisho wa nchi.

“Lengo la Chaneli hii ni kukuza Utalii wa nchi yetu hivyo ni lazima pia tukatangaza lugha yetu ya Kiswahili ambayo ni lugha kubwa duniani kwa sasa”Alisema Dkt. Mwakyembe.

Aidha Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Hamis Kingwangala ameeleza kuwa Channel hiyo inapaswa kuwa na wataalamu wa kutosha wenye uelewa mzuri wa kisayansi,wanaoelewa maisha ya wanyama pamoja vifaa vyenye teknolojia ya hali ya juu ili iweze kukidhi viwango vya kimataifa.

“Ni lazima kuwe na mawasiliano mazuri na utaratibu mzuri utakaoleweka katika urushwaji wa matangazo ili kuvutia watazamaji “Alisitiza Dkt.Kingwangala.

Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele amesema kuwa Chaneli hii ni lazima itambue soko ili iwe rahisi kuuza Utalii wetu pamoja na kuonyesha maeneo mengi ya nchi yenye vivutio mbalimbali.

Chaneli hiyo inatarajiwa kuanza kurusha matangazo yake katika majaribio ndani ya nchi mwanzoni mwa mwezi Disemba kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania TBC.