Katibu Mkuu Bi. Susan Mlawi Atembelea Kituo Cha Utamaduni Cha Pembenne Na Kufunga Kurugenzi Cup-Mbulu


Imewekwa 24th May, 2018

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ipo katika kuhakikisha inasimamia Utamaduni, kukuza michezo na kurejesha uzalendo hasa kwa vijana kwa ajili ya maendeleo ya jamii.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bibi.Susan Mlawi alipokuwa akiongea na Wananchi wa Kata ya Hydom Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu alipotembelea kituo cha Pembenne za Utamaduni (4CCP) ambako alipata fursa ya kuona ngoma za makabila mbalimbali ikiwemo Wadzabe, Wabantu, Waiiraq na Waakidatooga.

“Sisi kama Wizara inayosimamia Utamaduni tuna mikakati mbalimbali kuhakikisha tunalinda tamaduni hususani zile zinazoanza kupotea ”amesema katibu Mkuu Bibi. Susan

Alizidi kufafanua katika hotuba ya mwaka wa fedha 2018/2019 ya Wizara imeweka malengo ya kulinda lugha angalau nne ambazo zinaonekana kuanza kupotea.

Aidha Bibi. Susan alipata fursa ya kukagua na kushuhudia fainali za kombe la Kurugenzi lililoandaliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Bw. Hudson Kamoga lengo ikiwa ni kuhamasisha michezo.

“Kombe hili la Kurugenzi ni fursa mojawapo ya kuibua vipaji vya vijana ili kuweza kuwaendeleza na hivyo kukuza sekta ya michezo nchini” amesema Katibu Mkuu Bibi. Susan Mlawi,

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Bw. Hudson Kamoga alimshukuru Katibu Mkuu Bibi. Susan Mlawi kwa kuweza kufika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na kuweza kujionea fursa mbalimbali zilizopo Wilayani hapo ikiwemo Utamaduni na michezo.

“Fursa mojawapo uliyoishuhudia ni kuwepo kwa makundi manne ya lugha yanayopatikana Afrika ambapo Hydom ni sehemu pekee yenye fursa hii ya kipekee tofauti na sehemu nyingine ambapo utakuta lugha moja moja tu”amesema Mkurugenzi Kamoga.