Makatibu Wakuu kuonyesha uwezo wao wa kusakata kabumbu


Imewekwa 20th July, 2018

Makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali wataonyesha uwezo wao wa kusakata kabumbu siku ya Jumamosi ya tarehe 21 Julai 2018 katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma ikiwa ni maadhimisho ya Bonanza la michezo liloandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo.

Hayo yamesemwa jana Jijini hapo na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo wa Wizara hiyo Bw. Yusuph Singo ambapo ameeleza kuwa lengo la bonanza hilo ni kuhamasisha michezo kwa jaili ya afya pamoja na kuwakaribisha watumishi wa umma waliohamia Makao Makuu ya nchi .

“Katika bonanza hili mtashuhudia mechi kali itakayowahusisha Makatibu Wakuu wa Wizara zote za Serikali pamoja na Watumishi wa Umma wakichuana vikali” amesema Bw. Singo

Aidha aliongeza kwa kueleza kuwa mbali na fainali hizo kutakuwa na michezo ya ufunguzi ambayo ni mazoezi ya kutembea (jogging) ambayo yataanzia viwanja vya Jamhuri , kupitia Nyerere Square kuelekea mzunguko wa CDA (Round About)na kuhitimishwa katika viwanja vya Jamhuri.

Anazidi kufafanua kuwa baada ya mazoezi ya kutembea yatafuata mazoezi ya viungo (Aerobic) na baadaye mechi za ufunguzi ambazo ni mpira wa pete kati ya Watumishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Habari, na baadaye kufuatiwa na Makatibu Wakuu dhidi ya Watumishi wote.

Mechi nyingine ni mpira wa miguu kati ya Wizara ya Habari dhidi ya Ofisi ya Rais Utumishi, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Viwanda na Biashara , Kampuni ya Tigo na Kikundi cha Muungano na mwisho ni kati ya Makatibu Wakuu na Watumishi.

Bw Singo ameeleza kuwa mbali na kuhamasisha michezo pia Bonanza hilo linaunga mkono kauli mbiu ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kufanya mazoezi kwa afya.

Wananchi wa Dodoma wametakiwa kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia Bonanza hilo lililosheheni michezo mbalimbali itakayochezwa katika Bonanza hilo ikiwa ni kuamsha ari ya michezo kwa watumishi na wakazi wa Jiji la Dodoma.