Sekta ya Filamu ni Sekta Mtambuka - Dkt. Mwakyembe.


Imewekwa 15th November, 2018

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameeleza kuwa sekta ya filamu ni kiwanda mtambuka hasa katika uandaaji, urushwaji, uuzaji na usambazaji wa maudhui .

Hayo ameyasema leo Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa jukwaa la maudhui linalotarajiwa kufanyika Novemba 28 hadi 30 ,2018 Jijini Dar es Salaam.

“ Jukwaa hili lina umuhimu kwa kuimarisha maudhui na usambazaji uliobora kwa kiasi kikubwa katika kupata taarifa muhimu ikiwemo upatikanaji wa vifaa bora ili kuandaa kukidhi viwango vya kimataifa” amesema Dkt. Mwakyembe.

Amezidi kueleza kuwa kupitia jukwaa hilo litatoa fursa nzuri ikiwemo mijadala mbalimbali ya namna ya kutatua changamoto zinazowakabili waandaji wa maudhui wakiemo wa televisheni, redio pamoja na tasnia ya filamu .

Aidha Dkt. Mwakyembe ametoa rai kwa wadau mbalimbali wa filamu nchini kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika jukwaa hilo ili kutoa maoni yao kwa ajili ya kuboresha maudhui.

Naye Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kuwa maudhui bora yanasaidia katika kukuza lugha ya Kiswahili na kuongeza idadi ya vyombo vya habari vya mtandao vinavyosaidia katika kurusha matangazo hayo ndani na nje ya nchi.

Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza ameeleza kuwa Serikali iko tayari kuhakikisha inashirikiana na jukwaa la maudhui pamoja na wadau wote wa tasnia ya filamu ili kupata soko bora nje ya nchi.

Vilevile Mkurugenzi wa Uendeshaji wa kampuni ya Clouds Plus Production Bw. Ramadhani Bukini anafafanua kuwa uanzishwaji wa Jukwaa la Maudhui ni mpango wa kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji wa maudhui bora, kwa kutoa elimu kwa waandaaji na wasambazaji wa maudhui nchini.

Jukwaa la Maudhui linatarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam Novemba 28 hadi 30 , 2018 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo litahusisha midahalo na utoaji wa mada mbalimbali kutoka kwa wataalam waliobobea.