Serikali itaendelea kuwajengea uwezo wasanii kukuza soko la tasnia ya sanaa


Imewekwa 29th October, 2018

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amesema Serikali itaendelea kuwajengea uwezo, umahiri na ubunifu wasanii wa Tanzania kupitia Mradi wa Utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi (TASIP) ili kukuza soko la tasnia hiyo katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Akifunga Tamasha la 37 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani jana (Jumamosi Oktoba 27, 2018), Shonza alisema malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa tasnia ya sanaa nchini inapiga hatua kubwa zaidi na kuwafanya wasanii kunufaika na kazi zao.

Aliongeza kwa kuzingatia kuwa Wizara yake inasimamia na kutekeleza sera ya sanaa nchini, Serikali itahakikisha kuwa kuipitia mradi wa TASIP unawafikia na kuwatambua wasanii wote nchini na kuwawezesha kuwa na utambulisho rasmi utawaozesha kupata mitaji na mikopo ya kuendesha shughuli zao.

“Mwaka jana nilizindua mradi huu wa TASIP na mwaka huu tumeanza kushuhudia mafanikio makubwa kupitia program hii, kwa kuwa wapo baadhi ya wasanii waliotambuliwa na kusajiliwa na wameanza kupata mikopo kutoka mabenki hatua inayowezesha kupata kutatua baadhi ya changamoto katika kuendesha shughuli zao” alisema Shonza.

Naibu Waziri Shonza alisema Serikali itaendelea kutoa msukumo kwa wafadhili mbalimbali kuweza kuunga mkono Tamasha la Sanaa na Utamduni Bagamoyo linalofanyika kila mwaka nchini, kwa kuwa Tamasha hilo linawezesha wasanii wa Tanzania wanapata uzoefu wa masuala mbalimbali kutoka kwa wasanii wenzao wa mataifa mbalimbali ya nje na hivyo kuweza kuongeza ubunifu katika kazi zao.

Kwa mujibu wa Shonza alisema kwa kutambua umuhimu wa Tamasha hilo, Serikali itaendelea kuijengea Tasasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA) kwa ili kuwa na uwezo kuweza kuzalisha wasanii na wakufunzi wenye ubora katika ngazi ya kitaifa na kimataifa kwani Taasisi hiyo imekuwa kiungo muhimu cha uzalishaji wa wasanii katika mataifa mbalimbali ya kigeni.

“Tamasha hili limeongezaa mvuto wa Taasisi yetu ya TASUBA na kutangaza fursa na vivutio vilivyopo nchini na hivyo kudhihirisha kuwa Chuo chetu kina wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kukidhi soko la ndani na nje ya Tanzania, natoa rai kwa wasanii wetu kuendelea kujitokeza katika Tamasha lijalo na kutangaza uzalendo wetu” alisema Shonza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBA), George Yambesi alisema Tamasha la 37 limepata mafanikio makubwa kwa kuwa malengo yaliyowekwa na Taasisi hiyo yameweza kufikiwa na hivyo kuendelea kulifanya Tamasha hilo kuvutia wageni wengi zaidi kutoka nchi ya Tanzania.

“Wasanii wetu wameweza kuonesha Bidhaa bora zaidi zenye ushindani wa kitaifa na kimataifa, hivyo katika Tamasha lijalo tutahakikisha kuwa wasanii wetu wanakuja na bidhaa zilizokidhi ubora na ubunifu zaidi” alisema Yambesi.