SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA SHERIA, KANUNI NA MIKATABA YA TASNIA YA FILAMU


Imewekwa 05th October, 2017

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa serikali itaendelea kuboresha Sheria, kanuni pamoja na kushirikiana na bodi ya filamu kuandaa mikataba bora itakayoongoza tasnia ya filamu kuwa na mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi.

Hayo ameyasema jana Jijini Dar es Salaam aliposhiriki katika uzinduzi wa filamu mpya ijulikanayo kwa jina la BEI KALI na kuzitaka sekta mbalimbali za serikali kushirikiana na wasanii katika kujenga taifa bora kupitia tasnia ya filamu.

“Tasnia ya filamu nchini inakua, watanzania tupieni jicho kwenye filamu za bongo kuwaunga mkono vijana wengi wanaotumia tasnia hiyo kuonyesha uhalisia wa maisha mbalimbali yaliyomo ndani ya jamii zinazotuzunguka” amesema Mhe. Mwakyembe

Kwa upande wake katibu mtendaji bodi ya filamu Bibi. Joyce Fissoo amesema kuwa filamu ni uchumi, na uchumi hauwezi kuja bila ya jitihada hivyo kuwataka wanatasnia ya filamu kuzingatia uweledi kuanzia wanapotunga stori hadi katika kuuvaa uhusika ili kuziwezesha filamu za bongo kuonyesha uhalisia wa kile kilichokusudiwa.

Bibi. Fissoo amewapongeza waandaaji na washiriki wa filamu ya BEI KALI kwa kuuvaa uhusika na kuifanya filamu hiyo kurudisha heshima ya filamu nchini hivyo kuwataka watanzania kutopoteza nafasi ya kutafuta na kuona yale yaliyomo ndani ya filamu hiyo.

Naye Muhusika Mkuu katika Filamu ya BEI KALI Bw. Simon Mwapagata (Rado) amesema kuwa bongo movie haijafa kwani nyota haiwezi kung’aa bila ya kupata mwanga kutoka kwenye jua hivyo kuwaomba wadhamini kuendelea kujitokeza kudhamini na kuthamini filamu za bongo ili wasanii waendelee kutumia vipaji vyao kuelimisha, kuburudisha na kufikisha ujumbe katika jamii.

Aidha Bw. Mwapagata amewataka wasanii wa bongo movie kuwa na mshikamano na kuthamini kazi za kila msanii katika kuendeleza filamu za bongo na kuziwezesha kupendwa ndani na nje ya nchi.

Filamu ya BEI KALI iliyoshirikisha wasanii maarufu kama vile Simon Mwapagata (Rado), Irene Uwoya, Hemed Suleiman (Hemed Phd), Pacho Mwamba pamoja na wengine wengi imezinduliwa jana tarehe 4 oktoba 2017 na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa tasnia ya filamu nchini.