Serikali kuhifadhi Utamaduni wa Makabila yaliyo hatarini kupotea


Imewekwa 11th October, 2018

Serikali imejipanga kuanzisha programu ya kukusanya na kuhifadhi taarifa jamii za kitanzania ambazo asili ya utamaduni wake upo hatarini kupotea.

Kauli hiyo imetolewa leo katika Kijiji cha Hydom,Wilaya ya Mbulu Vijijini, Mkoani Manyara na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi alipokuwa akifunga Tamasha la Saba la Utamaduni wa Pembe Nne (7th Four Corner Cultural Festival) kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe ambaye ndiye alikuwa afunge tamasha hilo.

Bi.Mlawi alitoa pongezi kwa waandaaji wa tamasha hilo linahusisha makundi manne ya lugha yanayopatikana barani Afrika ila kwa Tanzania yanapatikana mkoani Manyara na jirani ambapo kwa sasa yameanza kupoteza asili yao na utamaduni wake ambayo ni Wahdzabe-Khoisan,Iraqw-Cushits,Datooga-Nilotic na Wabantu-Wanyiramba/ Wanyisanzu.

“Kupitia Idara ya Utamaduni iliyo chini ya Wizara hii nitaunda Kitengo kitakacho kuwa kinashughulikia suala la ukufanyaji wa taarifa za makabila mbalimbali nchini katika mfumo wa picha jongefu pamoja na uandishi wa historia fupi makabila hayo kwa lengo la kuweza kuhifadhi taarifa hizo kwa maslai ya vizazi vijavyo”alisema Bi.Mlawi.

Katibu Mkuu huyo aliendelea kueleza kuwa serikali inatambua changamoto ya utandawazi na elimu ambazo ni moja ya sababu ya baadhi ya tamaduni kuanza kupotea na katika hili serikali itasimamia kuendeleza tamaduni zile zilizo nzuri ila kwa zile zilizo mbaya kama ukeketaji kwa watoto wakike serikali itaendelea kupiga vita.