Serikali kuwaenzi Wanamichezo Wakongwe


Imewekwa 04th July, 2018

Serikali imeandaa mpango wa kuwaenzi watu mashughuri wakiemo wanamichezo wakongwe ambao wamewahi kuliletea taifa heshima katika mashindano mbalimbali akiwemo mwanariadha Mkongwe Bw. John Steven Akwhari.

Hayo yamesemwa leo Mbulu Mjini na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza alipomtembelea mwanariadha huyo nyumbani kwake ambapo alipata fursa ya kuona medani , tuzo na vikombe alivyowahi kushinda mwanariadha huyo.

“ Sisi kama Wizara tumeanzisha kampeni ya Uzalendo ambapo mwaka jana tuliwaenzi wasanii wa zamani wa muziki na mwaka huu mnamo Oktoba 14 ni zamu ya wanamichezo wakongwe akiwemo Bw. John Akwhari ” amesema Mhe. Shonza

Alizidi kueleza kuwa amevutiwa na jinsi mwanariadha huyo anavyotunza kumbukumbu zake huku akiwataka wanamichezo na watu wengine kuiga mfano huo bora ili kuviwezesha vizazi vijavyo kupata historia nzuri katika sekta ya michezo.

Naye Mwanariadha Mkongwe Bw. John Steven Akwhari amesema amefurahi kuona Serikali inatambua na kuthamini mchango wake katika sekta ya michezo na kuhaadi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kwa pamoja kuleta maendeleo katika sekkta hiyo muhimu.

Bw. John Akwhari ni mwanariadha wa zamani wa Tanzania wa kwanza kufungua milango ya kushiriki riadha nje ya nchi ambapo alijizolea umaarufu katika mashindano ya mwaka 1968 ya Olimpiki nchini Mexico ambapo licha ya kuwa wa mwisho aliueleza umati kuwa nchi yake ilimtuma kumaliza mbio na siyo kuanza mbio.