Timu ya JWTZ itayoshiriki Mashindano ya Wakuu wa Majeshi Bujumbura Kutumika Kuboresha Timu za Ndani Nchini.


Imewekwa 26th May, 2017

Wanamichezo watakaoteuliwa kuunda timu ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambayo itashiriki katika Mashindano ya Michezo ya Wakuu wa Majeshi nchini Burundi watatumika pia katika kuboresha timu mbalimbali ili kusaidia kuibua na kukuza vipaji vya michezo nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakati alipofungua Mashindano hayo kwa upande wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Dkt. Mwakyembe amesema kwamba, Mashindano hayo yanayohusisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo hufanyika kwa mzunguko miongoni mwa nchi wanachama yatakua chachu ya maendeleo katika sekta ya michezo kwani yatavumbua vipaji vingi katika michezo mbalimbali.

Amelipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuonyesha ushindani mkubwa katika mashindano mbalimbali ya Kitaifa na amewaomba wataalam kuendelea kuvumbua vipaji hivyo kwa manufaa ya vijana wa kitanzania na kuchukulia michezo kama sehemu ya kazi.

“Nachukua fursa hii kuzipongeza Kamandi zote kwa kuzingatia ushiriki wenu katika mashindano haya na kwa uzoefu wenu wa kuzingatia nidhamu ndiyo umekua msingi wa mashindano haya na mfano wa kuigwa katika mashindano mengine”, alisema Dkt. Mwakyembe.

Ameongeza kuwa, JWTZ kupiga hatua ya maendeleo katika michezo ni matokeo mazuri ya kuwekeza katika programu za kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo nchini, hivyo ametoa pongezi za dhati kwa kufanikiwa katika masuala ya michezo hususan mpira wa miguu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita Jeshini wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali Issa Nassor amesema kwamba, kupitia mashindano hayo vipaji mbalimbali vitaonekana na kuibuliwa na hivyo itasaidia kulipa sifa Taifa ndani na nje ya mipaka yake.

“Kwetu sisi wanajeshi michezo ni sehemu ya kazi, tumekua washiriki katika michezo mbalimbali na hii tunataka jamii iondoe ile dhana iliyojengeka kuwa eti sisi tuko kwa ajili ya vita na kutumia nguvu”, alisema Meja Jenerali Nassor.

Aidha, mashindano hayo kwa mwaka huu yanatarajiwa kufanyika mjini Bujumbura nchini Burundi mwezi Agosti ambapo Kaulimbiu ya Mashindano hayo ni “Shiriki michezo kama sehemu ya kazi, Kulinda Afya zetu na Kudumisha Mshikamano”, pia yatahusisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Huu utakuwa ni muhula wa nne kwa mashindano hayo kufanyika Afrika Mashariki ambapo timu ya JWTZ imekua ikifanya vizuri kwa kuchukua nafasi ya ya tatu kwa ujumla kati ya nchi zote zilizoshiriki katika mashindano yaliyofanyika hapo awali.