Vyama vya Michezo vyahimizwa kushirikiana na Serikali kutatua changamoto zilizopo.


Imewekwa 12th November, 2018

Serikali imevitaka vyama vya michezo nchini kushirikiana nayo katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika vyama hivyo ili kukuza michezo nchini.

Hayo yamesemwa leo Jiji Dodoma na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe wakati wa mashindano ya Dodoma Marathon yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini hapo.

“Ni lazima mshirikiane na Serikali katika kutatua changamoto pindi mnapokutana nazo lakini pia mnapotaka kuanzisha michezo kama hii, Wizara ipo tayari kushirikiana na nyie ili kuboresha panapohitajika marekebisho kwa manufaa ya maendeleo ya michezo hapa nchini” Alisema Dkt Mwakyembe.

Kwa upande wake mratibu wa mashindano hayo Bw.Ally Nchahaga alieleza kuwa lengo la kuandaa mashindano hayo ni kuendeleza vipaji vilivyopo katika riadha pamoja na kuendeleza juhudi za Serikali katika kukuza uchumi kupitia michezo.

“Lengo la Dodoma Marathoni ni kukuza vipaji vya riadha vilivyopo ili viendelee kujioneshana kujiuza kwakua michezo sasa hivi ni ajira kubwa sana ulimwenguni”Aliongeza Bw.Ally.

Ameongeza kuwa mbio hizo pia zinalenga kuitangaza Dodoma kama Makao Makuu ya nchi na kutaka wadau wengine waedelee kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza Jiji hilo.

Mbio hizo zilikua za Km. 42 na 21 kwa wanaume na wanawake pamoja na Km.2 na nusu kwa watoto na washindi mbalimbali walipata zawadi za fedha pamoja na medali.