Wabunifu mna nafasi kubwa kukuza Utamaduni Wetu:Dkt Mwakyembe.


Imewekwa 16th November, 2018

Serikali imewataka wabunifu kutumia vipaji pamoja na taaluma waliyonayo katika kukuza na kuutangaza Utamaduni wa nchi.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe alipokutana na Umoja wa mafundi Cherehani wa Jijini humo (UMACHEDO) ambapo amewataka watumie ubunifu walionao kutengeneza nguo zinazoitangaza nchi ili waweze kupata soko nje ya nchi.

“Wabunifu mnayo nafasi kubwa sana ya kutangaza Utamaduni wetu kupitia nguo mnazoshona,tumieni fursa hiyo ili mjitangaze vizuri ndani na nje ya nchi”Alisema Dkt. Mwakyembe.

Dkt. Mwakyembe ameendelea kuwasisitiza wabunifu hao kushirikiana na Serikali ili iweze kuwawezesha kwa kuwapa elimu ya namna ya kupata mitaji kupitia Taasisi za fedha pamoja na Taasisi zinazohusika katika uwezeshaji.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Sanaa Bibi. Leah Kihimbi aliwasisitiza wabunifu hao kujisajili katika Baraza la Sanaa La Taifa (BASATA) ili watambulike kama wasanii wa ufundi.

Naye Mshauri wa Umoja huo Bw.Christopher Mullemwa ameeleza kuwa umoja huo una lengo la kukuza uchumi wa pamoja na kuunga mkono Serikali ya awamu ya tano katika kauli mbiu yake ya Uchumi wa Viwanda.

Umoja huo una wanachama zaidi ya mia moja na unajishugulisha na kazi ya ushonaji.