Wadau wa Sekta ya Filamu Mkoani Songwe andaeni filamu za Kiutamaduni


Imewekwa 20th July, 2018

Wadau wa sekta ya Filamu Mkoa wa Songwe waelezwa kutumia fursa zilizoko Mkoani hapo ikiwemo uwepo wa maeneo mazuri ya asili naya kiutamaduni kwa ajili ya kuandaa filamu za Kiutamaduni.

Kauli hiyo imetolewa leo Wilayani Mbozi, Mjini Vwawa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw.Nicholaus William alipokuwa akifungua warsha ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya filamu mkoanI Songwe.

“Mkoa wa Songwe umebarikiwa kwa kuwa na fursa nyingi ikiwemo uwepo wa Kimondo ambacho ni kivutio kikubwa cha utalii pamoja na mandhari nzuri ya mkoa huu ambayo imekuwa ni kivutio kikubwa kwa wapiga picha wa kimataifa wanaokuja kupiga picha katika mkoa huu kwa ajili ya kuandaa Makala mbalimbali,”alisema Bw.William.

Akiendelea kuzungumza katika warsha hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa ni lazma kazi za filamu kuandaliwa kwa uweledi ili sekta ya filamu nchini iweze kushindana vyema na soko la filamu Afrika na Duniani kwa ujumla na kwa kuzingatia hilo filamu zenu zitaweza pia kushinda tuzo za kimataifa.

Kwa upande wa Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fissoo alitoa elimu kwa wadau hao wa filamu kwa kuwaeleza majukumu ya bodi ya filamu pamoja na kuwaeleza kuwa bodi ya filamu imekuwa ikitoa leseni na vitambulisho kwa ajili ya utambulisho wa wadau wanaojihusiha na kazi za filamu na hifadhi kanzi data ya wadau wa filamu nchini.

“Suala la ukaguzi wa kazi za filamu kwa mikoani kuanzia ngazi ya miswada inakaguliwa katika Halmashauri kupitia bodi zilizoundwa kupitia Afisa Utamaduni pamoja na wajumbe mbalimbali hivyo msanii wa mkoani mswada wa kazi yake ya filamu na filamu yake inakaguliwa nao na halazimiki kuja mpaka Dar es Salaam,”alisema Bibi Fissoo.

Pamoja na hayo Katibu Mtendaji huyo alieleza kuwa warsha hiyo itatoa mafunzo ya aina mbalimbali ikiwemo somo la Uandaaji wa Miswada ya Filamu,Somo la kijitangaza (Branding),Matumizi ya Mitandao na Matumizi ya lugha ya Kiswahili na masomo mengine yanayosaidia sekta ya filamu.

Mbali na hayo nae mmoja wa wasilishaji mada ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Filamu nchini Dkt. Vicenisia Shule aliwaeleza wadau hao wa filamu kuwa serikali inandaa Sera ya Filamu ambayo itasaidia kutoa mwongozo wa kuisimamia vyema sekta ya filamu kwa kuzingatia sheria inayosimamia sekta ya filamu nchini kwa sasa.

Hata hivyo warsha hiyo inatarajiwa kumalizika Julai,20 mwaka huu ambapo sherehe za ufungaji zitafanywa na Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza.