Washiriki wa mashindano ya Jumuiya ya Madola peperusheni vyama Bendera ya Tanzania


Imewekwa 27th February, 2018

Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza amewataka wanamichezo watakaoenda nchini Australia kushiriki mashindano ya jumuiya ya madola kutumia uwezo wao wa hali ya juu kwani wamepewa dhamana kubwa na nchi ya kupeperusha vyema bendera ya nchi katika mashindano hayo.

Rai hiyo ameitoa jana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla iliyoandaliwa na Balozi wa Australia nchini kuadhimisha ujio wa michezo ya jumuiya ya madola ya 21 itakayofanyika mwezi Aprili katika mji wa Gold Coast nchini Australia.

Mhe. Shonza amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wanamichezo wote nchini na kuwataka washiriki wa mashindano ya jumuiya ya madola kutoka Tanzania kuenzi mazuri yaliyowahi kufanywa na wachezaji wenzao katika mashindano hayo ya jumuiya ya madola.

“Ni faraja kubwa sana kwetu kwa kukaribishwa na mwenyeji wetu wa Australia, nikuhakikishie tu kuwa wachezaji wetu wamejiandaa vizuri na watashiriki vizuri na hata kuchukua medali katika mashindano hayo” amesema Mhe. Shonza

Kwa upande wake Balozi wa Australia nchini Tanzania Mhe. Alison Chartres amesema kuwa kwa mara ya kwanza mashindano ya jumuiya ya madola yatakuwa na medali sawasawa kwa jinsia zote na hii itasaidia kuongeza usawa na adhi ya jamii ili kupunguza ubaguzi ndani ya jamii na kuweka uwiano sawa.

Aidha Mhe. Chartres amewatakia kila la heri wachezaji kutoka Tanzania watakaoshiriki mashindano ya jumuiya ya madola kwa kuiwakilisha nchi vizuri kwani kila anayeenda katika mashindano hayo tayari ni mshindi kwa namna moja hivyo wachezaji watumie nafasi walizopata kushiriki mashindano hayo kuiletea sifa nchi ya Tanzania.

Timu kutoka Tanzania zitakazoshiriki katika mashindano ya jumuiya ya madola yatakayofanyika mwezi Aprili mwaka huu nchini Australia katika mji wa Gold Coast ni pamoja na timu ya mchezo wa Riadha, Timu ya mchezo wa mpira wa meza, Timu ya mchezo wa ngumi, pamoja na Timu ya mchezo wa kuogelea.