Washiriki wa Urembo Zingatieni Maadili na Utamaduni wa Kitanzania-Shonza


Imewekwa 07th July, 2018

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza ametoa wito kwa washiriki wa mashindano ya urembo nchini kuzingatia maadili na tamaduni za kitanzania kwa kuwa kielelezo bora kwa jamii .

Hayo ameyasema jana Jijini Arusha wakati wa shindano la kumtafuta mrembwende wa Jiji hilo , yaliyoandaliwa na The Function House chini ya uongozi wa Mkurugenzi Bw. Tilly Chizenga yaliyoshirikisha warembo 19.

“ Ninyi ni kioo cha jamii, mnaangaliwa na jamii nzima hivyo msibweteke mnapopata umaarufu bali muwe kielelezo bora cha utamaduni na maadili ya Kitanzania ” amesema Mhe. Juliana Shonza .

Anazidi kufafanua kuwa sanaa ya urembo ni ajira kama zilivyo ajira nyingine,na kuwaomba wazazi na jamii kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha mabinti wanatimiza ndoto zao katika sanaa hiyo.

Aidha ameeleza kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaojihusisha na vitendo vya unyanyasaji na uzalilishaji kwa washiriki wa mashindano hayo.

Vilevile alieleza kuwa tasnia hiyo iliingia doa ambapo kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja , Serikali ilisimamisha shughuli hizo kutokana na ubabaishaji na kukiukwa kwa taratibu na sheria za kuendesha mashindano hayo.

“Serikali ilichukua uamuzi wa kumfutia leseni muendeshaji wa awali, ila kwa sasa yamefunguliwa tena na jukumu hili linasimamiwa na Bi. Basila Mwanukuzi naamini tutaona mabadiliko mazuri katika tasnia hii” amesema Mhe. Shonza.

Naye Muandaaji wa Mashindano hayo Mkurugenzi wa The Fuction House Bw. Tilly Chizenga amesema kuwa maandalizi yalikuwa mazuri , ingawa kulikuwa na changamoto za hapa na pale .

Mashindano ya kumtafuta mrembo wa kuwakilisha Mkoa wa Arusha, yalishirikisha jumla ya warembo 19, ambapo Bi. Rukia Mhona aliibuka mshindi, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Bi. Teddy Mkenda na nafasi ya tatu imechukuliwa na Bi. Belinda Matemu washindi hao wote na wengine watatu wataungana na wenzao katika Kambi ya Miss Tanzania iliyopo Hoteli ya Serena Duluti Jijini hapo ili kumpata muwakilisha atakayewakilisha kanda ya Kaskazini katika mashindano ya Miss Tanzania.