Waziri Dkt. Mwakyembe awataka Waandishi wa Habari kuandika habari zenye utafiti wa kina.


Imewekwa 04th October, 2018

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa wito kwa waandishi wa habari kujikita zaidi katika kuandika habari zenye utafiti wa kina ili kuhabarisha jamii kwa taarifa zenye kujenga uelewa mzuri zaidi.

Hayo ameyasema jana Jijini Dar es Salaam katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Habari za maji kwa waandishi wa habari hizo ,zilizoandaliwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Shahidi .

“ Tuzo hii ni chachu na hamasa kubwa kwa waandishi wa habari nchini kujikita zaidi katika kuandika habari za maji ikiwemo utunzaji wa vyanzo vya maji”alisema Dkt. Mwakyembe

Aidha anatoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuhakikisha kuwa wanaweka maslahi mazuri kwa waajiriwa wao ili kuwapa ari ya kufanya kazi kwa bidii ikiwemo uandishi wa utafiti katika sekta mbalimbali .

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhe.Juma Uweso ameeleza kuwa maji ni muhimu katika kufikia dira ya maendeleo ya taifa ,hivyo kwa kuandika habari kuhusu maji zitasaidia jamii kupata uelewa wa kulinda na kutunza vyanzo vya maji .

“Ni muhimu kufahamu kuwa ni jukumu letu sote kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji ukizingatia maji ni uhai ” Alisema Mhe. Uweso

Alizidi kueleza kuwa Serikali ipo mstari wa mbele kuhakikisha inakabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo kwa kuweka mikakati thabiti ya kutumia vyombo vya habari katika kuelimisha umma umuhimu wa kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji.

Tuzo hizo za maji zilihusisha vipengele vitatu , ambapo kundi A lilihusisha mwandishi mahiri wa habari aliyetumia taarifa za mradi wa uhakika wa maji kuleta mabadiliko huku Bw. Sylvester Domasa akiibuka mshindi wa tuzo hiyo.

Kundi la pili lilihusisha uandishi mahiri wa habari za maji kwa uhakika wa Maji ambapo Bw. Nuzulack Dausen aliibuka mshindi, na kundi la mwisho lilikuwa linahusisha mwandishi mahiri wa habari za maji mwenye umri mdogo ambapo Amina Semagogwa kutoka Radio Kwizera aliibuka mshindi wa tuzo hiyo.

Tuzo hizo zimeandaliwa na Shirika la Shahidi wa Maji kupitia Programu ya Uhakika wa Maji kwa kushirikiana na Shirika la Water Witness International,WaterAid pamoja na Journalist Enviromental Association of Tanzania(JET).