Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amewasihi wanafunzi kushiriki katika michezo .


Imewekwa 11th June, 2018

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewasihi wanafunzi kushiriki katika michezo kwa ajili ya kukuza vipaji na kuimarisha afya zao pamoja na kusoma kwa bidii ili taifa liweze kupata wataalamu wazuri baadaye katika nyanja za michezo na elimu .

Hayo ameyasema leo Jijini Mwanza alipokuwa akifungua rasmi mashindano ya UMISSETA kwa shule za Sekondari nchini, yenye kauli mbiu ya “Michezo, Sanaa na Taaluma ni Msingi wa Maendeleo ya Mwanafunz katika taifa letu”.

“Kauli mbiu hii inamtaka mwanafunzi ajihusishe na michezo na sanaa kama sehemu ya taaluma ili kuonyesha vipaji vyao , ambavyo vikiendelezwa vyema vitaleta matokeo mazuri ikiwemo afya njema, taaluma bora na ajira”amesema Mhe.Kassim Majaliwa.

Anazidi kueleza kuwa suala la kukuza michezo nchini limepewa kipaumbele hivyo ni muhimu kwa kila mwannafunzi kutumia fursa ya mashindano hayo kucheza mchezo anaoupenda ili kukuza na kuendeleza kipaji alichonacho.

Aidha Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza Mikoa na Wilaya nchini kuhakikisha somo la haiba, michezo na stadi za kazi kwa shule za msingi linafundishwa kikamilifu, huku elimu ya michezo kwa shule za Sekondari ikitiliwa mkazo , pamoja na kuwaendeleza waliamu wa michezo kupitia vyuo mbalimbali nchini kikiwemo chuo cha Michezo Mallya.

Naye Naibu Waziri wa Habari ,Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza amesema kwa sasa Wizara iko katika mchakato wa kuhuisha sera ya michezo ya mwaka 1995 ili kuendana na mazingira halisi ya mabadiliko mbalimbali katika sekta hiyo.

“Sisi tukiwa Wizara inayosimamia sera ya michezo tutahakikisha tunaihuihisha sera hii ili iendane na mabadiliko yaliyomo katika sekta ya michezo nchini”amesema Mhe. Juliana Shonza.

Pia Mhe. Shonza anazidi kufafanua kuwa Mashindano ya UMISSETA yamekuwa ni chachu kubwa nchini, katika kuibua ,kuendeleza na kukuza vipaji vya vijana ambao baadaye wanaweza kuunda timu ya taifa na hivyo kuitangaza nchi sehemu mbalimbali kupitia michezo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara Ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amesema sekta ya michezo ni kiwanda kimojawapo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi hivyo ni vyema ikatiliwa mkazo kuanzia ngazi ya awali ili kupata wachezaji bora.

Mashindano ya UMISETA ni 39 kufanyika tangu yalipoanzishwa mwaka 1979 ambapo kwa miaka mitatu mfululizo Mwanza imekuwa mwenyeji ikihusisha wanafunzi wapatao 3892 kutoka mikoa 32huku miwili ikiwa ni Pemba na Unguja upande wa Tanzania Visiwani.