Waziri Mwakyembe atoa Miezi 3 kwa Maafisa Utamaduni kukamilisha ukusanyaji wa maoni ya Sera


Imewekwa 03rd September, 2018

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe amewataka Maafisa Utamaduni Mkoa na Wilaya kuwahimiza wadau wa Sekta ya Utamaduni kuwasilisha maoni yao ndani ya miezi mitatu.

Mheshimiwa Mwakyembe ametoa kauli hiyo leo katika Kijiji cha Marangu Mkoani Kilimanjaro alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Saba wa Umoja wa Machifu nchini wenye lengo la kujadili namna ya kuhakikisha umoja huo unasajiliwa kisheria pamoja na kuzungumzia nini kifanyike kutokana na kuwepo na mmomonyoko wa maadili katika jamii kwa kiasi kikubwa.

“Serikali iko katika mchakato wa kufanya maboresho ya Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 ambayo imeonekana kuwa na mapungufu kulingana na hali ilivyosasa,hivyo basi nitoe rai kwenu Machifu kama wadau wakuu wa Sekta ya Utamaduni kutoa maoni yenu kwa haraka kwani yatasaidia kwa asilimia kubwa kuongeza ubora katika sera hii tunayoboresha na hivyo basi hakikisheni mnawasilisha maoni yenu kwa Maafisa Utamaduni ndani ya miezi hiyo,”alisema Mhe.Dkt.Mwakyembe.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania Chifu Frank Marrialle alieleza kuwa umoja huo ulianza tangu mwaka 2014 na mpaka sasa unajumla ya wanachama 105 na kupitia umoja huo umekuwa ukisisitiza wajumbe wake kusimamia utunzaji mazingira pamoja usimamazi wa maadili katika jamii kwani machifu ndiyo mhimili wa kulinda utamaduni wa taifa.

“Mbali na Machifu hawa kujitahidi kupigania usimamizi wa maadili katika jamii zao wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi kwani kwa baadhi ya maeneo wamekuwa wakitolewa maneno ya dharau na kejeli kwa kuwaelezwa kuwa utawala wao umepitwa na hauna maana kwa sasa ombi letu kwa serikali ni kuhakikisha kupitia maoni yetu tutakayowasilisha kwa ajili Sera hii ya Utamaduni inayofanyiwa marekebisho yatiliwe mkazo ili kuonyesha wa nguvu ya machifu kwa jamii,”alisema Marrialle.

Aidha,akiendelea kuzungumza Chifu Marialle alipongeza uongozi wa serikali ya awamu ya tano kwa kusimamia utunzaji wa rasilimali za nchi kwa kuhakikisha hakuna utoroshwaji unaofanyika kwa lengo la taifa kupata faida itakayosaidia kuleta maendeleo nchini.

Pamoja na hayo nae Chifu Nshoma Hawa wa Ukamba - Kahama alitoa ombi lake kwa serikali la kuomba kusaidiwa kutokana na ikulu yake kuvamiwa na wanasiasa na kugaiwa kwa wananchi kwa matumizi ya kilimo kinyume na utaratibu wa himaya hiyo kwani eneo hilo ndipo walipozikwa machifu wote wa ukoo huo.

Halikadhalika nae Mlezi Mteule wa Umoja wa Machifu Tanzania Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.John Samuel Malecela alieleza kufurahishwa na uteuzi huo na kuahidi kushirikia na Machifu hao katika kuhakikisha Machifu hao wanafanikiwa kuleta maendeleo kwa taifa pamoja na kusimamia hali ya kupambana na mmomonyoko wa maadili uliyopo sasa kutokana na hali ya utandawazi.