Waziri Mwakyembe aunda Kamati ya kupitia Katiba ya Mchezo wa ngumi.


Imewekwa 04th January, 2018


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe ameunda kamati ya watu kumi na moja watakaopitia Katiba ya kusimamia mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini pamoja na kukusanya maoni namna bora ya kuendesha mchezo huo itakayoanza kazi kuanzia Januari 03 hadi 31 ambapo itakuwa chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) .

Akizungumza na wadau wa mchezo huo Jijini Dar es Salaam Mhe.Waziri ameiagiza Kamati hiyo kufanya kazi kwa pamoja katika kuunda mfumo mpya utakaolinda maslahi ya mabondia na wahusika wote wa mchezo huo ili kuleta heshima ya mchezo huo hapa nchini.

“Naomba mshirikiane katika kazi hii vunjeni makundi yenu ili mfanye kazi kwa maslahi ya Taifa na wanamasumbwi wetu,mkifanya hivyo tutaleta hamasa kubwa kwa watu wengi kujiunga na mchezo huu ambao unaleta ajira kwa vijana wetu”.Alisema Mhe.Waziri Mwakyembe.

Kamati hiyo itaongozwa na mwenyekiti Emmanueli Salehe ambaye ni mdau mkubwa wa ngumi hapa nchini,akisaidiwa na makamu Mwenyekiti Joe Enea ambaye ni Mwalimu wa ngumi pamoja na katibu Bw.Yahya Pori ambae pia ni mdau wa mchezo huo.

Wajumbe katika kamati hiyo ni Bw. Habibu A.Nyogoli mwanamasumbi wa zamani, Shomari Kimbau ambae ni muandaaji wa mapambano ya ngumi,Bw.Fike Wilson mwalimu wa ngumi,Bw.Anthony Ruta,mdau wa ngumi,Dkt.Killaga M.Killaga ambaye ni daktari wa wanamasumbwi hapa nchini.Wengine ni wanamasumbwi ambao ni Bw.Ally B Champion, Bw.Rashidi Matumla,na Bw.Karama Nyilawila ambao wameitangaza vyema nchi yetu katika mchezo huo.

Ameongeza kuwa katik kipindi hiki cha mpito shughuli za kutoa vibali kwa mapambano ya ndani na kwa mabondia wanaosafiri nje ya nchi zitaendelea kutekelezwa na BMTambapo ameiagiza BMT kuendelea kusimamia vibali vya safari za nje za mabondia kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za nchi.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Michezo (BMT) Bw.Mohamed Kiganja ameihakikishia kamati hiyo ushirikiano wa kutosha ili kutimiza adhma ya Serikali kuendeleza mchezo huo hapa nchini pamoja na kuwanufaisha wanamichezo hao.

Naye Bondia wa zamani Bw.Yassin Ustadh ameishukuru Serikali kwa kuamua kuunda Kamati hiyo ambapo amesema itaondoa migogoro mingi na ya muda mrefu iliyopo katika mchezo huo inayosababisha kupoteza hadhi yake na kutowanufaisha mabondia.