Waziri Mwakyembe azindua Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Michezo Malya


Imewekwa 15th May, 2018

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka wajumbe wa Bodi ya ushauri wa Chuo cha Michezo Malya kutumia kila aina ya ubunifu kuzigeuza changamoto zilizopo katika chuo hicho kuwa fursa ili kukipa chuo sura na nafasi yake stahiki kuwawezesha wahitimu kutambulika ndani na nje ya nchi.

Rai hiyo ameitoa wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ushauri jana katika Chuo cha Michezo Malya katika Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza na kusema kuwa Chuo cha Michezo Malya ni chuo cha pekee nchini hivyo hakina budi kuzalisha wataalamu wa kutosha wa kufundisha michezo katika shule, vyuo mbalimbali na hata katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Mwenyekiti na wajumbe wa bodi hii ni changamoto ya kwanza inayowakabili kuhakikisha kuwa taasisi hii yenye wajibu adhimu katika maendeleo ya michezo nchini mnaitangaza na kuiongezea thamani upya ili taasisi hii iweze sio tu kujulikana na watanzania bali vile vile ihudumie vijana wengi wenye ari kubwa ya kupata ujuzi katika michezo kutoka nchi mbalimbali” amesema Mhe. Mwakyembe

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Michezo Malya Mhandisi Dkt. Richard Masika amesma kuwa Bodi imedhamiria kufanya kazi kwa weledi, ubunifu uadilifu na bidii katika kushauri na kusimamia Chuo cha Michezo Malya ili kitekeleze ipasavyo maudhui na madhumuni ya kuanzishwa kwake.

Aidha Mhandisi Dkt. Masika amesema kuwa Chuo cha Michezo Malya ni dhana muhimu katika michezo kwa taifa letu kwani kinahitaji kuwa na wataalamu wa michezo wanaokidhi viwango vya taifa na vya kimataifa hivyo chuo kizingatie kuwa na wakufunzi mahiri, mitaala bora na mafunzo yenye ithibati

Kwa upande wake Mkurugenzi Maendeleo ya Michezo Bw. Yusuph Singo ametoa rai kwa wafanyakazi wa chuo cha Malya pamoja na wanachuo kuwapa ushirikiano bodi hiyo mpya ya ushauri ili baada ya miaka michache Chuo cha Michezo Malya kiweze kuvune mafanikio chanya yatakayokidhi mahitaji ya wakufunzi wa michezo ndani na nje ya nchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Eng. Mtemi Msafiri amewaomba Wajumbe wa bodi kuangalia namna ambavyo watawaunganisha wataalamu wanaopatikana kutoka katika Chuo cha Michezo Malya na wadau hususani Wizara ya Elimu na Tamisemi kwani wadau wote wanaotoka katika chuo hicho nia yao ni moja ya kukuza michezo nchini.