Wizara ya Habari yaandaa Mdahalo Kumuenzi Baba wa Taifa.


Imewekwa 12th October, 2018

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeandaa mdahalo maalum utakaohusisha mada mbalimbali katika kilele cha Kumbukuzi ya Kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwl.Julius K. Nyerere tarehe 14/10/2018 ili kumuenzi muasisi huyo.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Bibi. Leah Kihimbi amesema kuwa lengo la kuandaa mdahalo huo ni kumuenzi Baba wa Taifa kutokana na mchango wake mkubwa katika kuhamasisha Uzalendo nchini.

"Mdahalo huu ni muendelezo wa Kampeni yetu ya Uzalendo na Utaifa tunayoifanya kila mwaka ambayo kwa mwaka huu kilele chake kitakuwa ni tarehe 08 Disemba na kauli mbiu ya mwaka huu ni "Kiswahili Uhai wetu Utashi wetu" lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi kuwa Wazalendo kwa kutumia lugha yetu ya Kiswahili kwa ufasaha ili kulinda utamaduni wetu”, alisema Bibi Leah.

Aidha,amesema kuwa katika Mdahalo huo watalamu mbalimbali watawasilisha mada tofauti ikwemo Maisha na Uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere yanavyoakisi Uzalendo na Utaifa,Dhima ya Uzalendo na Utaifa katika maendeleo ya Uchumi na Viwanda pamoja na Mchango wa Kiswahili katika kukuza Uzalendo na Utaifa.

Kwa mujibu wa Bibi Leah, Mgeni Rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge na utafanyika katika ukumbi wa Chuo cha St.Johns Dodoma na utahudhuriwa na Viongozi na Wafanyakazi wa Wizara, Wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali pamoja na shule za mkoa huo na vikundi mbalimbali vya Michezo.

Mdahalo huo utakuwa ni sehemu ya Watanzania kutafakari,kubadilishana mawazo na kukumbushana kuhusu ulinzi wa Rasilimali za Taifa na uimarishaji wa misingi ya uzalendo na Utaifa.