Sisi ni Nani

Utangulizi

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba 1 la Januari, 2016. Katika kutekeleza majukumu yake kikamilifu, Wizara kimuundo imegawanyika katika maeneo makuu mawili;

USIMAMIZI NA UTEKELEZAJI WA MASUALA YA KISEKTA:

Eneo hili linatekelezwa na Idara ya Habari; Idara ya Maendeleo ya Utamaduni;Idara ya Sanaa na Idara ya Maendeleo ya Michezo kwa ushirikiano na Asasi zilizoko chini ya Idara hizo.

UENDESHAJI, URATIBU NA USIMAMIZI:

Eneo hili linatekelezwa na Idara ya Sera na Mipango; Idara ya Utawala na Rasilimali Watu; Kitengo cha Fedha na Uhasibu, Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani; Kitengo cha Mawasiliano Serikalini; Kitengo cha Ununuzi na Ugavi; Kitengo cha Huduma za Sheria na Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Kuendeleza utambulisho wa taifa kwa kuwezesha upatikanaji mzuri wa habari, kuwawezesha vijana kiuchumi, kukuza utamaduni na michezo kwa umma kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

MAJUKUMU YA WIZARA

Ili kufanikisha majukumu yake, Wizara inatekeleza Sera za Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Yafuatayo ni baadhi ya malengo yaliyoainishwa ndani ya Sera hizo:

SERA YA HABARI NA UTANGAZAJI YA MWAKA 2003

Kuweka mazingira yatakayowezesha sekta ya habari kukua.

Kuhamasisha vyombo vya habari kutoa huduma kwa kuzingatia maadili ya taaluma.

Kuhamasisha wanahabari kuendeleza chombo cha kujisimamia kitaaluma.

Kuweka utaratibu wa kujenga uwezo endelevu katika sekta ya habari.

Kuwawezesha wananchi kutoa na kupata habari kwa uhuru ili zichangie kuwaletea maendeleo.

SERA YA MAENDELEO YA UTAMADUNI YA MWAKA 1997

Kushirikisha shughuli za utamaduni wa taifa kuanzia shule za awali, sekondari na elimu ya juu na kuhakikisha kwamba mafunzo ya utamaduni yanaingizwa katika mitaala na mihtasari na kufundishwa shuleni na vyuoni.

Kuhimiza na kukuza utaifa kwa vijana wetu na wananchi kwa ujumla.

Kuhimiza utu katika maendeleo ya taifa.

Kuimarisha uchangiaji wa gharama, ukuzaji, utunzaji na uimarishaji wa taasisi za utamaduni kwa watumiaji wa huduma hizo.

Kuelimisha jamii juu ya masuala mbalimbali yanayohusu utamaduni na jinsi sanaa inavyoweza kutumika katika kupambana na UKIMWI.

SERA YA MAENDELEO YA MICHEZO YA MWAKA 1995

Kuhamasisha wananchi kushiriki michezo na mazoezi ya viungo vya mwili ili kuimarisha afya zao.

Kuhakikisha kuwa viwanja na vifaa bora kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya michezo vinapatikana.

Kuandaa na kutayarisha wataalamu katika fani na taaluma mbalimbali za michezo.

Kuhakikisha timu na wachezaji wetu wanashiriki kikamilifu katika mashindano na michezo ya kitaifa na kimataifa.

Kufanya utafiti wa michezo ya jadi kwa lengo la kuifufua na kuiendeleza.

Kuimarisha ushirikiano na mataifa mengine katika utoaji wa elimu kwa michezo na wanamichezo.

Kusimamia ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika Sekta ya Michezo.

Kuimarisha utawala bora katika michezo.

Kutoa mafunzo ya wataalamu wa michezo.

Kupambana na janga la UKIMWI katika michezo.

Kuendeleza na kutambua vipaji vya vijana katika michezo kuanzia umri mdogo.

ASASI ZILIZO CHINI YA WIZARA

SEKTA YA HABARI

• Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

• Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).

SEKTA YA MAENDELEO YA UTAMADUNI

• Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).

• Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).

• Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

• Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza Jukwaani.

SEKTA YA MAENDELEO YA MICHEZO

• Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

• Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.

• Vituo vya Michezo vya Arusha na Songea.